Mbuzi huyo aliyekuwa akimilikiwa na Julius Mawimbi, Mkazi wa Ukonga Mazizini, Dar es Salaam, ameibua maajabu mapya kwa namna alivyofikwa na mauti kisha kuzikwa mithili ya binadamu.
Imebainishwa kwamba Mawimbi alijulishwa kuhusu kifo cha mbuzi wake akiwa safarini, hivyo kwa mshangao, taratibu za mazishi zikaandaliwa, ikiwa ni pamoja na watu kukaa matanga.
Chanzo chetu cha habari kilisema Mawimbi aliporudi kutoka safarini, alichongesha jeneza la kuhifadhi mwili wa mbuzi huyo.
MAITI YA MBUZI IKAPANDISHWA NDEGE
Habari zinasema, mbuzi huyo aliwekwa kwenye jeneza na kusafirishwa mpaka Dodoma kwa ndege kisha kupelekwa nyumbani kwao, Mvumi ambako alizikwa.
Imeelezwa kuwa kifo cha mbuzi huyo, kimeiacha familia hiyo katika hali ya simanzi kwani wanafamilia walidai kuwa alikuwa ni msaada mkubwa kwao.
“Ni kweli mbuzi huyo alikuwa ni kama kioo ndani ya familia hiyo, kwa hiyo kifo chake ni pigo kwao,” kilisema chanzo.
Waandishi wetu walizungumza na mke wa Mawimbi ambaye alisema: “Mbuzi huyo alipokufa, mume wangu alikuwa safarini, hivyo tulipomtaarifu aliagiza tuweke matanga kama ambavyo binadamu hufanyiwa, tukafanya hivyo.
“Baada ya kurudi safari yake, alichukua jukumu la kumsafirisha kwa ndege hadi mkoani Dodoma kwa mazishi,” alisema mama Mawimbi.
Alibainisha kuwa mume wake alipomaliza mazishi ya mbuzi huyo, amekuja na tumbili, akaongeza: “Shughuli zilizokuwa zinafanywa na mbuzi aliyekufa sasa zitakuwa zinafanywa na tumbili huyo ambaye amempa jina la Dogo Janja,” alisema mama Mawimbi.
Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mazizini, Ukonga, Joseph Kabati alikiri kufahamu kifo cha mbuzi huyo kwani wakazi wengi wa Mazizini walikuwa wanamfahamu.
Mbuzi wa ajabu.
“Wengi walisikitishwa na kifo cha mbuzi huyo kwani alikuwa na matendo kama ya binadamu, alikuwa anakunywa bia, kula chapati na kadhalika, hali iliyofanya ajulikane kila kona ya mtaa wetu,“ alisema mwenyekiti huyo.
SOMA HABARI YA MBUZI HUYO ILIYOANDIKWA NA GAZETI LA AMANI LA AGOSTI 2 MWAKA JANA HAPA: MBUZI WA AJABU ASTAAJABISHA WATU DAR
chanzo ni GLOBARLPUBLISHERS
0 comments:
Post a Comment